Waziri Kairuki Afanya Ziara Dar, Kinondoni Kukagua Mradi Wa TASAF.......Asisitiza Waliotafuna Fedha Hizo Watatumbuliwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema atahakikisha anawachukulia hatua watendaji wote, walioshiriki katika udanganyifu wa kuingiza kaya zisizostahili katika Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Aidha, aliiagiza Tasaf kuhakikisha inafuatilia kaya zote ambazo ziliingizwa katika mpango huo bila kuwa na sifa zinazostahili, kwa kuziorodhesha kwa majina, wanapoishi na kiasi cha fedha walichopokea ili ripoti hiyo iwasilishwe kwa Rais John Magufuli.

Kairuki aliyasema hayo jana wakati akizungumza baada ya kupokea ripoti ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf III) ya Mkoa wa Dar es Salaam, sambamba na kuzungumza na wananchi katika mitaa ya Kigogo Kati na Mikoroshoni, Manispaa ya Kinondoni.

“Kaya ambazo hazistahili hawafanyi peke yao wanashirikiana na watu, kama ni viongozi katika ngazi za mitaa na kata mitaa tunataka majina, na katika kila jina tujue nani alishiriki kumuingiza nani alikuwa akimchukulia na kama yupo mtumishi wetu wa umma tujue ni nani na hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa.”
 “...Msije mkashangaa nikaja kuelekeza polisi kukamata hawa na hawa kwa sababu hizi hela ni lazima zirudi,” alisema Kairuki.

Alisema ameshapokea taarifa za mikoa mbalimbali, lakini Dar es Salaam na wilaya zake bado na mwisho ilikuwa ni Oktoba 6, mwaka huu, lakini aliwaongeza wiki moja ambayo tayari imeisha na orodha hiyo inatakiwa ipelekwe kwa Rais Magufuli.

Kairuki aliongeza kuwa pamoja na mkoa kusema umeondoa kaya 789 ambazo hazina sifa, lakini kuna kaya 5,457 ambazo zinapaswa kuondolewa katika mpango huo kwa kuwa hazina sifa za kupokea ruzuku hiyo. 
“...baada ya kuelekeza uhakiki wa nyumba kwa nyumba, sisi kwa taarifa tulizonazo tutaondoa kaya 5,457. Sasa ujiulize nyinyi ndio mlikuwa katika zoezi na mkapata idadi hiyo, hapa inaonesha kuna kitu hakipo sawa,” alisema.

Alisema katika kaya hizo zitakazoondolewa, 1,867 hazina vigezo vya umasikini, 563 zipo kwenye orodha lakini zilikuwa hazijitokezi kuchukua ruzuku na hazijulikani zilipo na kaya nyingine 2,114 hazikupatikana wala kujulikana zilipo wakati wa ukaguzi.

Alisema kaya hizi ni nyingi na hasa ikizingatiwa asilimia 76 hazijaingizwa katika mpango huo, hivyo kaya hizo ambazo ziliandikishwa zinapaswa kwenda kukaguliwa ili ziweze kuingizwa katika mpango huo ili katika awamu ya nane ya uhawilishaji fedha waweze kupata.

Kairuki alisema kiasi kikubwa cha fedha kimepotea, ambacho kingeweza kuwasaidia watu wanaostahili kuwa katika mpango huo. 
Alisema wilaya za Kinondoni na Temeke zimeshapokea malipo ya awamu saba ambayo ni Sh bilioni 6.7. Alisema hadi sasa kuna kaya 32,456 zilizoondolewa kwenye mpango huo.

Kwa wastani kaya moja hulipwa kati ya Sh 20,000 hadi 60,000 kwa kutegemea idadi ya watu katika kaya.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa alisema mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini kuna watu wanaoharibu taswira ya Tasaf.

Alisema kuna fedha nyingi ambazo zinaishia kwenye mikono ya wajanja na haziwafikii walengwa wa mpango huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema mpango huo umeandaliwa kitaalamu na utaendelea kuwa endelevu na kwamba mradi huo unategemea zaidi serikali na wafadhili, lakini hadi sasa kiasi kikubwa kimekuwa kikitoka kwa wafadhili.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala bora Mh. Angela Kairukia akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,akiendelea na ziara katika Mkoa wa Dar es salaam kukagua maendeleo ya mradi wa kusaidia kaya masikini TASAF

0 comments:

Post a Comment