Watafiti
hao waliuawa juzi kwa kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa
moto. Gari la Serikali aina ya Toyota Hillux, pia lilichomwa moto.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba wanawashikilia watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa
kijiji.
Alisema
mwenyekiti wa kitongoji alipigiwa simu na mmoja wa wanawake waliokuwa
eneo la tukio kwamba kuna wanyonya damu wamevamia kijiji.
Mambosasa
alisema kwa kuwa mwenyekiti huyo alikuwa mbali, alimpigia simu
mwenyekiti wa kijiji aende eneo la tukio kujua kilichotokea. Alisema
mwenyekiti wa kijiji alipofika hakuamini maelezo ya watafiti hao na
kuanza kuwashambulia.
Mambosasa
alisema mtu mwingine alikwenda kijijini na kumueleza mchungaji wa
kanisa kuhusu kijiji kuvamiwa na nyonya damu, naye akatagaza kwenye
kipaza sauti kwamba kijiji kimevamia na watu hao.
Alisema wanakijiji walijitokeza kwenda eneo la tukio na kuwashambulia watafiti hao hadi kufa.
Mkuu
wa Mkoa, Jordan Rugimbana alisema baada ya kutembelea eneo la tukio,
ameamua kuwasimamisha kazi kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino
na ofisa utumishi wa wilaya hiyo kwa madai ya kutosambaza barua za
kuwatambulisha watafiti hao katika maeneo waliyokwenda kufanya kazi.
Mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Simon Kawea alisema taarifa alizozipata kutoka kwa
diwani wa kata ya Iringa-Mvumi, watafiti hao walipofika katika eneo la
Makamwa walikutana na watu na kuwauliza kilipo kijiji cha Iringa-Mvumi.
Kawea alisema watafiti hao walipofika eneo walilotaka kufanya utafiti walipigiwa yowe kwamba ni wanyonya damu.
Alisema
baada ya kelele zile wanakijiji waliokuwa katika mkutano walisikia na
kutoka na mapanga na silaha za jadi kisha kuwavamia watafiti hao na
kuwashambulia kwa silaha hizo.
“Hata
walipoonyesha vielelezo wao si wezi bali ni watafiti waliopewa kibali
na halmashauri ya Chamwino na vielelezo vingine, wanakijiji walikataa na
kuendelea kuwapiga,” alisema.
Alisema
watendaji wa kijiji hicho na diwani wa kata hiyo, Robert Chikole
waliwasihi wanakijiji kuwaacha watafiti hao lakini walizidiwa nguvu na
wananchi.
Aliongeza: “Hata
polisi walifika muda mfupi, walikuta wameumizwa vibaya wakarusha risasi
juu lakini walizidiwa nguvu na kukaa pembeni. Kwa kweli wamekufa katika
tukio la kinyama,” alisema.
Alisema
watafiti hao walikwenda katika ofisi za Wilaya ya Chamwino na kupata
kibali kabla ya kwenda kijijini hapo kwa ajili ya kufanya utafiti wa
udongo.
Alisema diwani, mtendaji na mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Habari kutoka kijijini hapo zinasema wanakijiji wamekimbia makazi yao kutokana na msako wa polisi kwenye eneo hilo.
Majonzi yatawala Arusha
Mauaji
ya hayo yameibua simanzi katika taasisi ya Selian na familia zao,
ikiwamo ya mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk January Mfuru ambaye mtoto
wake pia ameuawa.
Mtoto huyo, Faraji Mafuru amehitimu Chuo cha Mipango Dodoma hivi karibuni na alikuwa katika mazoezi kwa vitendo.
Mratibu
wa utafiti katika kituo hicho, Dk Charles Lyamchai alisema tukio hilo
limetokea wakati timu ya watafiti wa kituo hicho ikiwa mkoani Dodoma
kutekeleza mradi wa kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya kuziingiza
kwenye kanzidata ya Taifa.
“Hawa
walikuwa kwenye mradi maalumu ambao umeanza mwaka 2014 na wapo wengine
watafiti ambao wamesambaa kwenda mkoani Dodoma kwa kazi hii,” alisema.
Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni dereva Nicas Magazine na Mtafiti wa maabara ya udongo, Teddy Lumanga.
“Wapo
watumishi 10 huko kutoka hapa kituoni, waliokwenda kutekeleza mradi wa
kutambua kiwango cha rutuba kwenye udongo nchini ambao tumeshaukamilisha
kwenye wilaya zote za mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Katavi na wilaya
ya Kondoa, hili ni jambo la kushtua sana,” alisema.
Alisema
watafiti hao walikuwa katika wiki ya pili na hawakuwa wamepata matatizo
yeyote tangu wafike Dodoma, baada ya tukio hilo kiongozi wa msafara
aliwasiliana na kituo.
Dk
Lyamchai alisema kabla ya kwenda huwa wanatoa taarifa kwa kuandika
barua kwenye wilaya husika, pia maeneo ya vijijini huwa wanaambatana na
mabwana shamba.
“Watafiti
wetu hawana mahusiano yoyote na masuala ya damu, walikuwa kwenye kazi
zao na walitoa taarifa hadi ofisi ya kata ila hatujui ni kwa nini tukio
hili limejitokeza,” alisema.
Mtafiti
mwandamizi wa kituo hicho, Dk Lameck Makoye alisema hawajawahi kukutana
na changamoto kubwa kama hiyo hasa maeneo ambayo huwa na historia ya
wenyeji wasiopenda wageni.
Alisema
Dk Mafuru na watafiti wengine waliondoka jana kwendas Dodoma kuungana
na watafiti wengine kutoka Kituo cha Hombolo na Makutupola kwenda eneo
la tukio.
Selian
ni miongoni mwa vituo maarufu katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na
Kati kwa kufanya tafiti za mazao katika maeneo yenye ukame nchini.
0 comments:
Post a Comment