WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan
Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw
Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala
ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Magereza
mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza
madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa
gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawa moja
limegharimu sh. 70,000.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 5, 2016 wakati alipotembelea
Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo
yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.
Alisema
kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa
nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo
amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000
kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.
“Nimesikia
kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji
wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia
shughuli za Serikali,” alisisitiza.
Serikali
imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa
kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwemo
madawati ili kuyaongezea tija aliongeza
Kwa
upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi alisema
waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.
Aidha,
Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha
ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo
katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Kuhusu
changamoto ya makazi kwa askari Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua
na imeweka mkakati wa wa ujenzi na kwa upande wa askari Magereza
wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu alitembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali
zikiwemo nguo katika maeneo ya soko la Sabasaba na Majengo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment