Mapokezi makubwa yaliyopangwa kufanyika leo jijini Dar es salaam ya
kuwapokea Wajumbe wa Baraza Kuu la CUF na Kamati ya Uongozi ya chama na
Katibu Mkuu Maalim Seif yameota mbawa kufuatia kusitishwa kwa hofu ya kutokuwepo usalama.
Mapema
jana, ilitangazwa kwamba Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad, wajumbe wa baraza kuu la CUF na kamati ya uongozi ya chama
wangefanyiwa mapokezi makubwa katika ofisi hizo lakini yaliahirishwa
ghafla baadaye usiku kwa kuhofia kuwapo vurugu.
Kiongozi
wa wabunge wa CUF waliokuwa wameandaa mapokezi hayo, Riziki Shahari
alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wameahirisha
mapokezi hayo baada ya kujiridhisha kuwa hali ya usalama siyo nzuri.
“Tunazo
taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya ofisi huku
yakilindwa na vyombo vya dola tangu ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa
mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.
“Tunajipa
muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba
wanachama wote walioko Dar, mikoani na Zanzibar wawe watulivu kwani
chama kina viongozi makini na hawawezi kuwa tayari kuona maisha ya
wanachana na viongozi yanahatarishwa kwa kuigeuza ofisi kuu kuwa uwanja
wa mapambano,” alisema Shahari.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema wabunge 41 kati ya
43 wa CUF walioandaa mapokezi hayo walikuwa wamekwishafika Dar es
Salaam, lakini wamechunguza na kubaini kuwa yangeleta maafa.
Hata
hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema
pamoja na hayo, chama hicho kimeshamalizana na Profesa Lipumba na
kusisitiza kuwa si mwanachama tena.
0 comments:
Post a Comment