ATCL Kuanza na Kosa la Kwanza


ATCL kama yalivyo mashirika mengine ya umma, kila mara imekuwa ikizaliwa na kufa kutokana na muundo wake usiokuwa wa kibiashara. TANESCO isiyo na mshindani yeyote, TTCL ambayo awali haikuwa na mshindani, na mengine mengi yaliyokwishakufa na yaliyouzwa, mashirika yote hayo yalikufa kwa sababu yalianzishwa, kuendeshwa na kusimamiwa kiserikali/kisiasa.

Serikali haijawahi kuendesha biashara ikafanikiwa. Tatizo linaanzia kwenye muundo wa haya mashirika/makampuni. Wanasiasa/viongozi wa serikali ambao kimsingi si wafanyabiashara ndiyo waliotengeneza muundo wa uendeshaji na ndiyo wenye kauli ya mwisho. Vigezo vya wajumbe wa bodi na watendaji wakuu wanavyo wao. Na siku hizi PhD imekuwa ni kigezo kikubwa sana ingawa kiuhalisia, kwa Dunia nzima, ni nadra sana kuwaona wenye PhD wakiwa wafanyabiashara wazuri na waliofanikiwa.

Juzi wakati Mh. Rais akizindua ujio wa ndege mpya alisema ATCL imezaliwa upya, ina ndege mpya, bodi mpya na uongozi mpya, sikusikia kama ina muundo mpya wa uendeshaji na usimamizi. Bado inaonekana ATCL itandeshwa kwa mkono wa serikali.

RAIS - 'ATCL ISITUMIE MAWAKALA WA KUKATISHA TIKETI'

Hili tayari ni agizo ambalo naamini ni agizo lisilo sahihi. Tayari serikali imeanza toka hatua za mwanzo kuingilia uendeshaji wa ATCL. Rais anapoagiza ATCL isitumie mawakala wa kukatisha tiketi inamaanisha ATCL iwe na wafanyakazi waajiriwa kila mahali nchini. Gharama za maelekezo hayo itakuwa kama ifuatavyo:
ATCL italazimika kuwalipa wakatisha tiketi mishahara, matibabu, posho, michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, usafiri, n.k. ATCL italazimika kulipia gharama hizo zote bila ya kujali mkatisha tiketi anakatisha tiketi ngapi au kama amepata wateja au hakupata kabisa
ATCL italazimika kulipia ofisi na kuweka miundombinu ya ukatishaji ticket nchi nzima. Ifahamike kuwa ukitaka kuwa na ufanisi unalazimika kuwa na ofisi za ukatishaji tiketi hata mahali ambapo ndege haitui, kwaajili ya kuhudumia abiria wanaotoka maeneo hayo wanaotarajia kutumia usafiri wa ATCL kutokea uwanja ulio karibu
ATCL italazimika kuwapa mafunzo wakatisha ticket watakaotapakaa nchi nzima
Wakati ATCL watakapokuwa wanahangaika na kuwa na wakatisha ticket wao na ofisi zao, washindani wao wataendelea kuwa na wafanyakazi wachache, wakiwa na mawakala wengi wanaolipwa kutokana na idadi ya ticket na thamani ya ticket walizokatisha. Hawalipii ofisi, hawalipii matibabu, hawalipii michango ya hifadhi ya jamii, hawalipii likizo ya mfanyakazi. Mawakala wao wanalipwa kutokana na wanachozalisha, wasipozalisha hawalipwi chochote.

ATCL wanaanza na quandary ya kwanza, wafuate maagizo ya mwenye mali au kanuni za biashara? Je, hii ni ya mwanzo na ya mwisho au zitaendelea kuja na nyingine? Kwa kuwa tatizo la msingi la uendeshaji biashara zilizo chini ya serikali halijatatuliwa, haitakuwa jambo la ajabu ATCL kufuata projectile ya mashirika/makampuni ya umma.

By Msambichaka Mkinga

0 comments:

Post a Comment