UTAFITI Twaweza ‘Wambeba’ Tena Magufuli

RIPOTI ya utafiti mpya wa taasisi ya Twaweza imeeleza kuwa watanzania wengi wanaunga mkono, hatua ya Rais John Magufuli kupiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa hapa nchini, anaandika Aisha Amran.

Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,602 kati ya tarehe 23 na 29 Agosti, mwaka huu kwa njia ya simu. Utafiti huo ulihusisha wananchi wa Tanzania Bara pekee na kwamba watu 6 kati ya 10 wamepinga kuwa nchi inaongozwa kidikteta.

Watu hao ni sawa na asilimia 58, walipinga kuwa nchi inaongozwa kidikteta huku asilimia 31 wakieleza kutokuwa na uhakika juu ya suala hilo.

Katika utafiti huo unaopewa jina la, “Demokrasia, udikteta na maandamano” unaripoti kwamba  asilimia 80 ya watanzania waliohojiwa, wanasema  baada ya uchaguzi, vyama vya upinzani vikubali kushindwa na visaidiane na serikali kuijenga nchi.

Huku asilimia 20 pekee ndiyo wananchi wakisema wapinzani waifuatilie na kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo imedaia kuwa asilimia 71 ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanaunga mkono kufanyika kwa mikutano huku asilimia 37 ya wafuasi wa chama tawala nao wakiunga mkono kufanyika kwa mikutano ya hadhara.

Aidha ripoti hiyo ya Twaweza inadai kuwa, asilimia 48 ya waliohojiwa juu ya kuanzishwa harakati za Umoja wa Kupinga Udikteta (UKUTA), wanapinga umoja huo huku asilimia 22 pekee wakiunga mkono umoja huo.

Pia asilimia 55 ya wafuasi wa vyama vya upinzani waliohojiwa, wanaunga mkono harakati za umoja huo huku asilimia 44 wakiwa hawaungi mkono na asilimia 6 ya wafuasi wa CCM wanaunga mkono juhudi za Ukuta.

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, amesema watanzania wengi wanaunga mkono mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni.

“Hili ni jambo la kuzingatiwa na serikali kwa sasa, wananchi ya hawakubaliani na kauli inayosema kuwa Rais Magufuli ni dikteta, wanasema ili kulinda amani  na kuchochea kasi kubwa ya maendeleo lazima hatua thabiti zichukuliwe,” amesema Eyakuze.

0 comments:

Post a Comment