Profesa Tibaijuka alitoa taarifa hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alisema tuzo hiyo ya Maendeleo Endelevu ilidhaminiwa na mwana Mfalme wa Bahrain, Khalifa bin Salman Al Khalifa.
Alisema, hatua ya kuzikataa fedha hizo, ni njia ya kukwepa mtego kama uliomkuta mwaka juzi baada ya kupokea fedha za Escrow Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mfanyabiashara, James Rugemalira.
Tuzo hiyo ambayo ni heshima kwa Tanzania, alikabidhiwa Septemba 24, mwaka huu na inajulikana kama ‘His Royal Highness Prince Khalifa bin Salman Al Khalifa Award for Sustainable Development’.
Profesa Tibaijuka alisema, alikabidhiwa tuzo hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha maendeleo duniani.
Alisema tuzo hiyo ya heshima hutolewa kila baada ya miaka miwili na washiriki wakuu huwa ni wale waliowahi kufanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa.
Mwaka huu, Waziri Mkuu wa Bahrain Khalifa bin Salman ndiye aliyemkabidhi tuzo hiyo, alisema.
“Tuzo hii nimepewa Marekani ikiwa kama sehemu ya kutambua mchangoa wangu katika kuhamasisha maendeleo na nilikabidhiwa katika Makao Makuu ya UN na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali duniani.
“Na huambatana na zawadi ya Dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 200). Sikuzichukua fedha hizi, kama mnavyojua maadili ya nchi yetu unaweza ukapokea yakaibuka mambo mengine.
“Ingawa kwenye ule mkutano niliwaambia kuwa sipokei fedha kutokana na hali halisi … niliwaambia kuwa kama mnavyojua katika mkoa ninaotoka (Kagera) kuna tetemeko limetokea,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema kupokea tuzo hizo si kwa ajili ya mafanikio yake binafsi bali kwa Watanzania wakiwamo wapiga kura wake wa Muleba Kusini ambao muda wote wamekuwa wakimtia moyo wa kufanyakazi kwa bidii.
Profesa Tibaijuka ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema ameuachia Umoja wa Mataifa (UN) na wadhamini wa tuzo hiyo waamue cha kufanya kuhusu fedha hizo.
Katika kupokea tuzo hiyo, mbunge huyo alisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe (CCM).
0 comments:
Post a Comment